Salamu - Septemba, 2026

Bwana Yesu Kristo asifiwe sana. Karibu sana katika salamu za mwezi huu wa tisa.

Katika mwezi uliopita tulikuwa na semina katika mkoa wa Songwe, pale Tunduma mjini. Tulikuwa na semina nzuri sana katika kumaliza mwezi wa nane.

Asanteni kwa maombi yenu na sadaka zenu mlizotoa kwa ajili ya kujenga ufalme wa Mungu.

Nina kuletea salamu za mwezi huu wa tisa — karibu sana tujifunze. Kumbuka tuna salamu zenye kichwa:

JIFUNZE KUTAKA KARAMA AU KUOMBA MUNGU AKUPE KARAMA YA MIUJIZA NA UPONYAJI (SEHEMU YA PILI)

Hebu tusogee mbele kidogo.

7: MUNGU ANAWEZA KUTUMIA MIUJIZA ILI WATU WABADILIKE TABIA AU WAMGEUKIE

Sikia: Mungu anapoona watu wake wakiwa mbali naye na wamebanwa sana katika eneo la akili zao, anaweza kutumia miujiza ili watu hao wamfuate Mungu.

Angalia mifano hii michache:

“44 Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi. 45 Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko.” (Luka 24:44–45)

Sikia kuhusu kufunua akili: fahamu akili hiyo ilikuwa imefunikwa. Jambo la kufunulia akili ni muujiza — si jambo la kawaida. Fikiri: hawa ndugu walikuwa na shida ya kuelewa; ghafla Mungu akawafanya waanze kuelewa. Hili si jambo la kawaida.

Unajua, ukiwaona watu wengi wanaabudu sanamu na mambo kama hayo, fahamu shida ipo katika akili au ufahamu. Ukiwaona watu wasiomjua Mungu, fahamu shida ipo katika akili. Mungu, ili awasaidie hao watu kuelewa, anaweza kutumia muujiza ili akili zao zikae sawa na wamgeukie Mungu.

Angalia mfano huu mwingine:

“36 Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. 37 Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. 38 Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. 39 Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, BWANA ndiye Mungu, BWANA ndiye Mungu.” (1 Wafalme 18:36–39)

Kwa mujibu wa mistari hii, utaona kuwa muujiza wa moto kushuka, ulipoonekana, uliwafanya watu wote waliokuwa mbali na Mungu wamrudie Mungu, wamwangukie, na kumwabudu tena.

Hata leo ndivyo hivyo. Mwanadamu anapoona muujiza, ndipo anapomgeukia Mungu.

Angalia mfano huu mwingine:

“2 Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. 3 Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. 4 BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.” (Kutoka 3:2–4)

Kilichomfanya Musa amgeukie Mungu ni muujiza aliyouona wa kijiti kikiwaka moto lakini hakikuteketea. Musa aliouona muujiza huo akageuka. Sikia: muujiza unamfanya mtu ageuke. Kama alikuwa mbali na Mungu, muujiza unamfanya ageuke na kuuangalia muujiza.

Kama muujiza huo umetoka kwa Mungu, ni rahisi mtu anayeona muujiza aanze kumwangalia Mungu aliye ndani ya muujiza huo.

Kumbuka: kile kijiti kilipowaka moto na hakikuteketea, ndani yake Mungu alikuwa na lengo la kukutana na kuzungumza na Musa. Musa alikuwa mbali na Mungu; muujiza huo ulimvuta Musa ili atazame vizuri.

Mungu alipomuona Musa amegeuka ili aone, ndipo Mungu akamwita. Musa alipoitwa, akaitika. Kumbuka: sauti ile ilitokea katikati ya kijiti kinachowaka.

Sikia: ili leo hii watu wamrudie Mungu, tunahitaji kuzijua mbinu mbalimbali. Moja ya mbinu ni hii ya karama ya miujiza. Angalia mfano: karama ya uponyaji wa kimiujiza inapofanya kazi, ndipo watu wengi humgeukia Mungu.

Si unakumbuka muujiza wa watu elfu tano (wanaume, nje ya hesabu ya wanawake na watoto) kwa mikate michache na samaki wachache?

“22 Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng’ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja, tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao. 23 (Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru.) 24 Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. 25 Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa? 26 Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 27 Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu. 28 Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu? 29 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.” (Yohana 6:22–29)

Kwa mujibu wa mistari hii, utajifunza kuwa muujiza wa ulaji wa mikate na samaki uliwafanya watu wamtafute Mungu na wamtumikie au watende kazi za Mungu.

Bwana Yesu Kristo alijua kuwa kilichowafanya watu wamgeukie ni muujiza wa kula mikate. Bwana Yesu Kristo aliwaambia wazi kuwa muujiza ule ndiyo uliowafanya watu hao wamtafute au wamgeukie Mungu.

Hebu tujifunze kuitaka karama hiyo ya miujiza na karama ya uponyaji.

Mungu akubariki sana.


Ukihitaji masomo yetu, unaweza kuyapata kwa njia zifuatazo:

1. App yetu ya huduma yenye jina “HUSONEMU (MWAKATWILA)” — inapatikana Play Store, ambapo kuna masomo mengi sana.

2. Tovuti yetu: www.mwakatwila.org

3. YouTube: HUDUMA YA SOMA NENO LA MUNGU

4. Facebook: ingia kwenye tovuti yetu uone alama ya Facebook (f), kisha “like” ili upate maelezo ya kujiunga, au tafuta “SOMA NENO LA MUNGU”

5. Instagram: tafuta “Huduma ya Soma Neno la Mungu”

6. DVDs 📀 au CDs 💿

7. Vitabu

NB: Wasiliana na mhudumu ofisini kwa namba +255 763 109 733 ili kupata vitabu, DVD na CD.

8. Kwa njia ya redio:

  • Rungwe FM 102.5 MHz — Jumapili saa 3:00 hadi 4:00 usiku
  • Baraka FM 107.7 MHz — Jumanne saa 12:00 jioni hadi 1:00 usiku
  • Bomba FM 104.1 MHz — Ijumaa saa 3:00 hadi 4:00 usiku

9. Online Radio: radio.mwakatwila.org

Ratiba ya vipindi:

  • Saa 12:00 asubuhi
  • Saa 07:00 mchana
  • Saa 12:00 jioni
  • Saa 03:00 usiku

10. Ingia MWAKATWILA YouTube Online

Kwa mawasiliano zaidi:

+255 754 849 924
+255 756 715 222

Wako,
Mwl. Steven Mwakatwila & Beth Mwakatwila